Wednesday, September 10, 2014

WAPENZI WA JINSIA MOJA WAFUNGA NDOA BAADA YA KUISHI PAMOJA MIAKA 72




Zaidi ya miongo sabini baada ya kuanza uhusiano wa kimapenzi, Vivian Boyack na Alice "Nonie" Dubes wamefunga ndoa.
Boyack, 91, na Dubes, 90, walifunga ndoa rasmi Jumamosi iliyopita, limeripoti gazeti la Quad City Times.
"Sherehe hii ilikuwa ifanyike siku nyingi sana," amesema mchungaji Linda Hunsaker wakati akifungisha ndoa hiyo iliyohudhuriwa na marafiki wachache na baadhi ya wanafamilia wa maharusi.
Wawili hao walikutana katika mji waliokulia wa Yale, Iowa, nchini Marekani. Baadaye walihamia mji wa Davenport mwaka 1947, Boyack akifanya kazi ya ualimu, huku Dubes akifanya shughuli za kihasibu.
Dubes amesema wameishi maisha mazuri pamoja, katika miaka yote hiyo na wameweza kutembelea majimbo yote 50 ya Marekani, na ya Canada, na pia kutembelea Uingereza mara mbili.
"Tumekuwa na wakati mzuri," amesema Dubes.
Boyack amesema inahitaji mapenzi ya dhati na kujituma kuweza kuendeleza penzi kwa miaka 72.
Rafiki wao wa muda mrefu Jerry Yeast, 73, amesema alikutana nao zamani wakati akifanya kazi nyumbani kwao akiwa kijana mdogo.
"Nimewafahamu wanawake hawa maisha yangu yote, na ninakwambia, ni wa kipekee," Yeast amesema.
Jimbo la Iowa lilianza kuruhusu ndoa za wapenzi wa jinsia moja mwaka 2009. Wanawake hao wamesema hawajachelewa kuanza ukurasa mpya katika maisha yao.
(Taarifa na picha kutoka The Guardian)



No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...